Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali nchini Libya si muafaka kwa wakimbizi na wahamiaji-UNHCR na IOM

Hali nchini Libya si muafaka kwa wakimbizi na wahamiaji-UNHCR na IOM

Kabla ya mkutano rasmi wa Muungano wa Ulaya mjini Valletta nchini Malta hapo kesho Ijumaa, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na la kimtaifa la uhamiaji IOM wametoa wito kwa viongozi wa Ulaya kuchukua hatua thabiti kushughulikia tishio la kupotea kwa maisha katika bahari ya Mediterranea na mazingira mabaya kwa wahamiaji na wakimbizi nchini Libya.

Katika taarifa yao ya pamoja wamesema kuwa ili kulinda wakimbizi na wahamiaji, Umoja wa Ulaya unahitaji kuwa imara zaidi ndani na nje ya mipaka yake, kusaidia na kutafuta suluhisho kwa watu wenye mahitaji. Hii ni pamoja na kujenga uwezo wa kuokoa maisha katika bahari au nchini, kuimarisha utawala wa sheria na vita dhidi ya mitandao ya kihalifu.

Wametoa wito kwa juhudi za pamoja ili kuhakikisha kuweko kwa uhamiaji endelevu na mifumo ya ukimbizi nchini Libya wakati kuna usalama na hali ya kisiasa na pia katika nchi jirani.

Mashirika hayo mawili yameomba kuondolewa kwa hali ya kuwaweka kizuizini moja kwa moja wakimbizi na badala yake kuundwa huduma stahiki za mapokezi na kuwapa mazingira salama na ya heshima, ikiwa ni pamoja na kwa watoto.