Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani shambulio dhidi ya watendaji wake Afrika Magharibi

UM walaani shambulio dhidi ya watendaji wake Afrika Magharibi

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali shambulio dhidi ya ujumbe wake karibu na mpaka wa Nigeria na Cameroon, shambulio lililosababisha kuuawa kwa watu watano akiwemo mkandarasi huru wa umoja huo.

Yaelezwa kuwa shambulio hilo lilitokea Jumatatu karibu na eneo la Kontcha nchini Cameroon wakati wajumbe wa timu hiyo inayofuatilia mzozo wa mpaka kati ya nchi mbili hizo walipokuwa kwenye majukumu yao.

Katika taarifa yao, wajumbe wa Baraza la Usalama wametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa na serikali za Nigeria na Cameroon.

Wamesisitiza kuwa vitendo vya ugaidi ni tishio kwa amani na usalama duniani hivyo wametaka wapangaji, wafadhili na watekelezaji wafikishwe mbele ya sheria.

Wametoa wito kwa serikali hizo kuchunguza mara mojra shambulio hilo na wahusika wafikishwe mbele ya sheria huku wakisihi usalama uimarishwe kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wengine wanaofanya kazi kwenye maeneo hayo.