Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maisha katika vifusi ndio hali halisi Homs-Grandi

Maisha katika vifusi ndio hali halisi Homs-Grandi

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi ameshuhudia kile alichosema ni janga kubwa la mahitaji ya kibindamu jijini Homs nchini Syria.

Katika ziara yake nchini humo kwa mara ya kwanza, Grandi ametembelea majengo na maeneo yaliyoharibiwa na kuteketezwa na vita vilivyomalizika mwezi Aprili mwaka 2014 katika mji huo mkongwe..na kusema

(Sauti ya Grandi)

"Tazama uharibifu huu, uharibifu wa vita hivi, hii ndio sababu ya wakimbizi kutoka Syria, ambao wanakataliwa kuingia nchi zingine, hii ndio sababu na kitu ambacho wakimbizi hawa wamevikimbia."

Vile vile ametembelea makazi yanayowahifadhi watu waliopoteza nyumba zao, na kusema ...

(Sauti ya Grandi)

"Ni lazima kwanza tufikirie kwamba kuna watu hapa, baadhi yao wanarejea katika magofu haya, wanahitaji msaada, msaada wa haraka, wanasikia baridi, wana njaa, wanahitaji kufanya kazi kupata kipato, wanahitaji vifaa vya msingi, na tunahitaji kuharakisha misaada ya kibinadamu, tunahitaji rasilimali kwa hilo".

Amesema ujenzi wa mji ulioharibiwa kwa miaka minne utachukua muda, lakini kujenga maisha ya watu walioathiriwa na vita, hilo ni jambo kubwa mno.