Skip to main content

Zuio la wakimbizi kwa misingi ya kibaguzi si suluhu ya ugaidi- Guterres

Zuio la wakimbizi kwa misingi ya kibaguzi si suluhu ya ugaidi- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres amezungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani na kusema mikakati baguzi ya kudhibiti ugaidi inachochea vikundi vya kigaidi kuibuka na mikakati mipya zaidi ya kutekeleza shughuli zao.

Amesema hayo alipoulizwa swali iwapo anaona agizo la Rais Donald Trump wa Marekani la kuzuia raia kutoka nchi saba kuingia Marekani kama njia muafaka ya kudhibiti ugaidi.

(Sauti ya Guterres)

“Iwapo kikundi cha kigaidi kitajaribu kushambulia nchi yoyote kama vile Marekani, bila shaka hawatakuja na hati za kusafiria kutoka nchi zenye migogoro hivi sasa. Wanaweza kuja hati za kusafiria za nchi zilizoendelea zaidi au wanaweza kutumia watu ambao wameishi miongo kadhaa ndani ya nchi.”

 Na kuhusu mwelekeo wa mazungumzo kati ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Marekani wakati huu ambapo inaonekana kuchukua msimamo tofauti juu ya ushirikiano wa kimataifa, Guterres amesema mambo magumu yana majibu rahisi..

(Sauti ya Guterres)

“Na jibu ni tuwe thabiti kwenye kutathmini misingi yetu na kuwa wazi tunaposhiriki kwenye kwenye mazungumzo fanisi. Ni mchanganyiko huu ambao ndio nitajaribu kuuimarisha tunapozungumza na Marekani au serikali yoyote ile duniani.”

Awali alielezea mafanikio kutokana na ushiriki wake kwenye mkutano wa viongozi wa wakuu wa nchi za Muungano wa AFrika, AU huko Addis Ababa, Ethiopia ambapo amezungumzia makubaliano kuhusu utekelezaji wa ajenda 2030 na ile 2063 ya Afrika kuhusu maendeleo.

(Sauti ya Guterres)

“Kutakuwepo na ushirikiano kamilifu kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika kuhusu malengo ya maendeleo endelevu na mkataba wa tabianchi wa Paris katika miaka ijayo.”

Halikadhalika amesema Kenya imekubali kushiriki katika jeshi la kikanda la Afrika litakalokwenda kulinda amani Sudan Kusini na kwamba wamekubaliana kila mwaka wakati wa mkutano wa viongozi wa AU mwezi Januari, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atashiriki kikao maalum na viongozi wa Afrika kutathmini ushirikiano kati ya vyombo hivyo.