Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Udhibiti wa mipaka kwa misingi ya rangi, kabila utaifa haufai- Guterres

Udhibiti wa mipaka kwa misingi ya rangi, kabila utaifa haufai- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres amesema ingawa nchi zina haki na wajibu wa kulinda mipaka yao dhidi ya vikundi vya kigaidi, mipango hiyo haipaswi kutekekelezwa kwa misingi ya kidini, kabila au utaifa.

Katika taarifa yake iliyosomwa na msemaji wake, Stephane Dujarric mbele ya wanahabari, Katibu Mkuu amesema fikra hizo zinamjia wakati akirejea kutoka Ethiopia nchi ambayo inaongoza kwa hifadhi kubwa ya wakimbizi barani Afrika licha ya hatari za usalama ambazo hukumbana nazo.

Hivyo amesema mipango ya aina hiyo ya udhibiti haifai kwa sababu..

(Sauti ya Dujarric)

 “Ni kinyume na maadili ya kimsingi yanayounda jamii zetu,na kwa kuwa inaibua hofu na chuki vinavyoweza kurahisisha  propaganda za vikundi vya kigaidi ambavyo sote tunataka kukabiliana navyo. Hatua za upofu zisizotokana na intelijensia thabiti zinaonekana hazifai kwa kuwa zinaweza kuvukwa na vikundi vya kigaidi duniani ambavyo zama za leo ni vya aina yake.”

image
Wakimbizi na wahamiaji wakisubiri kushuka kutoka meli ya wanamaji ya Italia ili waingie kwenye meli nyingine itakayowafikisha mji wa Pozallo. (Picha:UNHCR/Francesco Malavolta)
Bwana Guterres amesema ana hofu kubwa kuwa hatua hizo kote duniani zimekuwa zinafubaza maadili ya mfumo wa kimataifa wa kulinda wakimbizi.

(Sauti ya Dujarric)

“Wakimbizi wanaokimbia mapigano na mateso wanakuta mipaka mingi zaidi imefungwa na vikwazo vingi kupata ulinzi na huduma wanazohitaji kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya mkimbizi.”