Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yakabidhi jengo jipya la hospitali DRC

MONUSCO yakabidhi jengo jipya la hospitali DRC

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO umekabidhi jengo jipya la hospitali ya rufaa ya Erengeti huko jimbo la Beni.

Makabidhiano hayo yanafuatia ujenzi uliofanywa na MONUSCO baada ya shambulizi la tarehe 29 na 30 mwezi Novemba mwaka 2015 ambapo wagonjwa na wahudumu wa afya waliuawa na jengo kuteketezwa kwa moto.

Akikabidhi ufunguo wa jengo hilo, Mkurugenzi wa ofisi ya MONUSCO huko Béni-Butembo-Lubero, Warner Ten Kate amesema hospitali hiyo ya rufaa sasa ina vifaa vya kisasa vya kupiga picha kufuatilia ujauzito, halikadhalika gari la wagonjwa linaloweza kuwapeleka hospitali kuu ya Oicha au Komanda.

Ufadhili wa jengo hilo pamoja na vifaa vya tiba na dawa ni sehemu ya mipango ya MONUSCO ya miradi yenye matukio ya haraka na umegharibi dola 150,700.

Kila mwezi hospitali hiyo ya Erengeti hupokea na kulaza wagonjwa 350.