Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutaendelea kuwa bega kwa bega na Tanzania- Guterres

Tutaendelea kuwa bega kwa bega na Tanzania- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres amemhakikishia Rais John Magufuli wa Tanzania ushirikiano kutoka chombo hicho ikiwemo usaidizi kwenye tatizo la wakimbizi.

Bwana Guterres ametoa hakikisho hilo wakati wa mazungumzo kati yao, kando mwa mkutano wa wakuu wa Muungano wa Afrika, AU huko Addis Ababa, Ethiopia.

Amesema Umoja wa Mataifa utatia msisitizo zaidi katika kuhimiza wadau mbali mbali wa maendeleo wa jumuiya ya kimataifa kuchangia juhudi zinazofanywa na Tanzania za kuwapatia hifadhi wakimbizi wa nchi mbalimbali tangu mwaka 1971.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameelezea juhudi za Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki za kushughulikia mzozo wa Burundi, akisema harakati hizo zinazoongozwa na Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa zinaendelea vizuri.