Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ombi WHO na Iraq la vifaa vya matibabu Mosul laitikiwa

Ombi WHO na Iraq la vifaa vya matibabu Mosul laitikiwa

Ombi la shirika la afya duniani, WHO la usaidizi wa vifaa vya matibabu huko Mosul, nchini Iraq limepata jibu baada ya serikali ya Ufaransa kuwasilisha vifaa hivyo ikiwemo dawa na vile vya upasuaji.

Mwakilishi wa WHO nchini Iraq, Altaf Musani amesema usaidizi huo kupitia mfumo wa usaidizi wa raia wa Muungano wa Ulaya, utawezesha matibabu kwa majeruhi wengi wanaotoka Mashariki mwa Mosul.

Ametaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na vikasha 20 vya vifaa vya upasuaji vinavyotosha kufanya upasuaji 2,000 pamoja na dawa za kuokoa maisha zinazotosheleza wagonwa 12,000, ambapo nusu vinapelekwa hospitali mbili kuu za rufaa mjini Erbil, kaskazini mwa Iraq.

Bwana Musani amesema mapigano huko Iraq yamesababisha makovu ya mwili na kifikra huku majeruhi wanawake, wanaume, wasichana na wavulana wakisimulia madhila ambayo hata wao hawajawahi kuyasikia.

Hivyo amesema msaada huo kutoka Ufaransa umekuja wakati muafaka na kiashiria cha ubinadamu.