Skip to main content

Suluhu ya kisiasa pekee ndio itainusuru Sudan Kusini:UM,AU na IGAD

Suluhu ya kisiasa pekee ndio itainusuru Sudan Kusini:UM,AU na IGAD

sudankusiniSuluhu ya kisiasa pekee kwa kuzingatia muafaka wa amani wa mwaka 2015 ndio itainusuru Sudan Kusini ambayo sasa imeghubikwa na machafuko, mauaji na ukatili mwingine.

Kauli hiyo imetolewa kwenye mkutano wa pamoja kuhusu Sudan Kusini, wa Umoja wa Mataifa, Muungano wa Afrika AU na IGAD, uliofanyika Jumapili Januari 29 kandoni na mkutano wa Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia.

image
Mkutano huo ulioongozwa na mwenyekiti Hailemariam Desalegn, waziri mkuu wa Ethiopia na mwenyekiti wa IGAD, umehudhuriwa pia na mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Mwakilishi wa AU Sudan Kusini Rais wa zamani Alpha Oumar Konare, na mwenyekiti wa tume ya pamoja ya uangalizi na tathimini (JMEC), Rais wa zamani Festus Mogae.

Wengine walioshiriki ni waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia, katibu mkuu wa IGAD, Kamishina wa amani na usalama wa AU na maafisa wengine wa ngazi ya juu kutoka mashirika hayo matatu.

image
AU, IGAD na Umoja wa Mataifa wameelezea hofu yao kuhusu kuendelea kwa machafuko na hatari ya vita hivyo vya kijamii kusababisha uasi na mauaji ya watu wengi, na pia hali mbaya ya kibinadamu Sudan Kusini.

Mashirika hayo pia yamesisitiza kuendelea na jukumu lao la pamoja la kusaka amani ya kudumu , usalama na utulivu katika taifa hilo changa. Wamerejelea wito wao wa kusitishwa haraka uhasama na kuzitaka pande zote kuhakikisha ujumuishwaji wa mchakato wa kisiasa , katika majadala wa kitaifa uliopendekezwa na katika utekelezaji wa makubaliano ya amani.

AU, IGAD na Umoja wa Mataifa wameahidi kuimarisha ushirikiano wao kwa kuunga mkono mchakato wa amani wa Sudan Kusini.