Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumeongeza huduma za dharura kukabiliana na majeruhi Mosul-WHO

Tumeongeza huduma za dharura kukabiliana na majeruhi Mosul-WHO

Ikiwa migogoro wa ndani ya Mosul nchini Iraq inaongezeka na idadi kubwa ya raia kujikuta katikati ya mapigano hayo, shirika la afya duniani WHO na washirika wake wameongeza huduma za dharura wanazotoa ili kuhakikisha kwamba wagonjwa wanaohitaji huduma za matibabu kwa majeruhi wanazipata na kuna nafasi kubwa ya kuishi.

Hata hivyo fedha zaidi zinahitajika ili kutoa huduma za afya kamili kwa watu milioni 2.7 walioathirika. Taarifa hiyo ya WHO imesema kuwa bado kuna viwango vya juu vya visa vya mahututi karibu na maeneo ya mapigano ambapo kesi nyingi zinahitaji rufaa kutoka Mosul hadi Erbil kaskazini mwa Iraq.

Inasemekana kuwa tangu Oktoba 17 mwaka jana hadi Januari 18 mwaka huu raia 1610 raia waliojeruhiwa walipelekwa kwenye hospitali kuu ya Erbil kupokea huduma za wagonjwa mahtuti. Hospitali nyingi Mosul zimeharibiwa na hazina uwezo wa kutoa huduma za afya kwa watu wa kawaida na raia wanaojeruhiwa ambapo wagonjwa wanaendelea kupata matatizo makubwa na baadhi yao kupoteza maisha. Dkt Wael Hatahit afisa wa operesheni za dharura wa WHO Iraq amesema

(Sauti ya Dr. Wael Hatahit)

"Kwa sababu ya operesheni za kijeshi, kesi nyingi tunazozipeleka mjini Erbil, na muda tunaochukua kati ya Mosul na Erbil karibu saa nne kwa sababu ya vituo vya ukaguzi, hii inasababisha vifo vya wagonjwa mahututi na wanapofika huwa wako kwenye hali mbaya sana. Kwa hivyo kuwepo kwa hospitali kwa dakika ishirini kutoka Mosul inasaidia sana kupunguza idadi ya vifo au hata kesi za mahututi. Tukichelewa inaweza kusababisha matokeo mabaya ambayo si tu kupoteza maisha mara nyingi kiungo cha mwili kukatwa."

Ili kuziba pengo hili, WHO na washirika wake wameanzisha hospitali yenye vitanda eneo la Bartella, mashariki mwa Mosul. Na hospitali nyingine tatu za ziada zenye uwezo wa kuwa na vitanda 40-50 zitaanzishwa haraka iwezekanavyo magharibi na kusini mwa Mosul. WHO imeweka magari ya wagonjwa 36 tayari, na kliniki 30 ili kufikia wagonjwa. Pia imetoa vifaa vya upasuaji kwa wagonjwa 3100 wanaohitaji huduma ya upasuaji.