Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusisahau machungu ya wahanga wa Holocaust-Guterres

Tusisahau machungu ya wahanga wa Holocaust-Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amesema ulimwengu utafanya kosa kubwa ikiwa utadhani kuwa mauaji ya halaiki dhidi ya wayahudi ni matokeo tu ya ujinga wa kundi la kihalifu la manazi.

Guterres amesema hayo leo wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya wahanga wa mauaji ya halaiki yenye maudhui "mustakhbali bora unategemea elimu".

Amesema dunia ina wajibu wa kukumbuka mauaji ya halaiki yaliyofanywa kwa kukapangwa kwa lengo la kutokomeza jamii ya wayahudi na wengine wengi.

(Sauti ya Gutteres- 1)

"Mauaji ya halaiki yalikuwa ni kilele cha chuki, visingizio na ubaguzi dhidi ya wayahudi, jambo tunaloita sasa chuki dhidi ya wayahudi. Cha kusikitisha na kinyume cha azma ya kutatua, chuki dhidi ya wayahudi inaendelea kushamiri. Tunashuhudia pia ongezeko la misimamo mikali, chuki dhidi ya wageni, ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya waislamu. Ukosefu wa fikra sahihi na stahmala vinarejea."

Akinukuu azimio la haki za binadamu na katiba ya Umoja wa Mataifa amesema kamwe dunia hatuwezi kukaa kimya pindi tunaposhuhudia chuki na machungu dhidi ya mwadamu, na hivyo akatoa ahadi..

(Sauti ya Gutteres- 2)

"Mimi nawahakikishia kuwa kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nitakuwa mstari wa mbele kupiga vita chuki dhidi ya wayahudi na aina nyingine zote za chuki."

Wakati huo huo mmoja wa waathirika Elie Buzyn mwenye umri wa miaka 90 anakumbuka hasa hofu na mateso mikononi mwa Manazi na kusema...

(Sauti ya Elie)

"Unaweza kusema kwamba wakati huu, lakini zaidi ya hilo, tishio la wakati ujao, kwani kila kitu kinaweza kuanza tena kwa njia tofauti lakini pengine hata kwa ukatili zaidi , hasa leo na silaha za maangamizi. zinaweza kusababisha uharibifu hata mkubwa kuliko vita vya dunia vya 1939-1945 "