Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madhila Syria yanatisha, imegeuka kama machinjioni - OCHA

Madhila Syria yanatisha, imegeuka kama machinjioni - OCHA

Mwaka wa jana 2016 raia wa Syria walishuhudia uharibifu na mateso makubwa yasio na kifani, hii ni kwa mujibu wa mratibu wa masuala ya dharura wa Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien akizungumza kwenye Baraza la usalama hii leo hap makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwenye mkutano kuhusu Mashariki ya Kati ukiangazia Syria.

Bwana O’Brien ameelezea masikitisho yake kuhusu majanga yanayozidi kuendelea nchini Syria, raia wamepoteza maisha yao na huduma za misaada haziwafikii walioathirika akitoa wito kwa Baraza la Usalama kuhakikisha kuwa juhudi za kusitisha mapigano zinatiliwa maanani. Ameongeza kuwa mkutano uliofanyika hivi karibuni Astana wa wapinzani kuweka kando silaha zao ni jambo la kuleta matumaini kwa juhudi za kutafuta suluhisho la kisiasa.

Ikiwa mgogoro wa Syria unaingia mwaka wa sita, Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu wanne kati ya watano nchini Syria sasa wanaishi katika umaskini wakighubikwa na madhila

(Sauti ya O’Brien)

"Bado tunasikitishwa na ripoti za watoa misaada ya kibinadamu kuingiliwa wakiwa kazini, tumeona uharibifu mkubwa kwa maeneo ya Darrya na maeneo mengine, miji kuharibiwa, kulipuliwa na mabomu na raia kufukuzwa, mabasi ya kutoa misaada ya kibinadamu yakichomwa, katibu mkuu, mimi na wenzangu tumeyaiita tuliyoshuhudia machinjio, bila utu na ubinadamu."

Hata hivyo Bwana O’Brien ameongezea kuwa kuna matumaini

(Sauti ya O’Brien)

"Tunaanza mwaka wa 2017 japokuwa kumekuwa na mateso, kuna matumaini kuna sitisho la mapigano kwa taifa japokuwa kuna changamoto za hapa na pale, hii inatupatia fursa sote tuweke juhudi zaidi ili kuiendeleza."