Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen nuru inazidi kutoweka, chukueni hatua- O’Brien

Yemen nuru inazidi kutoweka, chukueni hatua- O’Brien

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo wamejulishwa kuwa hali ya kibinadamu nchini Yemen imezidi kudorora huku mapigano yakizidi kushika kasi kila uchao iwe makombora ya angani au mashambulizi  ya ardhini.

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa kibinadamu, OCHA, Stephen O’Brien ametolea mfano wiki iliyopita pekee ambapo wamepokea ripoti ya matukio 365 ya mapigano ikiwa ni ongezeko toka 231 wiki iliyotangulia.

Amesema matukio hayo ni kwenye jimbo la Taizz pekee akisema ni dhahiri kuwa mashambulizi yanayoendelea yanawadhuru raia wasio na hatia.

Wakati huu ambapo zaidi ya theluthi mbili ya wananchi wa Yemen wanahitaji msaada, nuru kwa watoto ikizidi kuyoyoma, Bwana O’Brien pamoja na mambo mengine ametoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Usalama akisema..

(Sauti ya O’Brien)

‘Watumie ushahiwi wao kwa pande husika kwenye mzozo kuhakikisha sheria za kimataifa za kibinadamu zinazingatiwa na kutoa fursa kwa misaada ya kibinadamu kuweza kufikia wahusika bila vikwazo vyovyote.”

Halikadhalika ametaka kuwezesha utoaji mikopo kwa wafanyabiashara na benki nchini Yemen ili kufanikisha ununuzi wa vyakula vya msingi ikiwemo ngano.