Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wagombea watatu wa Ukurugenzi Mkuu wa WHO wanadi sera

Wagombea watatu wa Ukurugenzi Mkuu wa WHO wanadi sera

Shirika la afya ulimwenguni WHO, limesema idadi ya waliosalia kwenye kinyang’anyiro cha Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo sasa imefikia watatu baada ya mchujo kutoka wagombea watano.

Watatu hao wanawania kuchukua nafasi ya Margret Chan anayemaliza muda wake tarehe 30 Juni mwaka huu ambapo uchaguzi wa mrithi wake utafanyika mwezi Mei mwaka huu.

Mjini Geneva, Uswisi wagombea wa nafasi hiyo ambao ni Dk Tedros Ghebryeesus wa Ethiopia, David Nabarro wa Uingereza na Dk Sania Nishtar wa Pakistan wamenadi sera zao mbele ya waandishi wa habari na kisha kuulizwa maswali na wanahabari na watu wengine waliojiunga kwa njia ya simu.

Wagombea wote hao kila mmoja ameeleza uzoefu wake katika masula ya afya kitaifa na kimataifa na kisha kutaja vipaumbele vyao ikiwa watachaguliwa.

Mgombea pekee mwanamke Dk Sania Nishtar amesema kipaumbele chake ni katika lengo na muundo wa WHO.

image
Picha:WHO/Video capture
( Sauti Dk Nishtar)

‘’Kipengele cha kwanza katika maono yangu ni kurejesha ahadi ya WHO na kuhakikisha inapata imani kama shirika la afya linaloongoza, na kujikita katika mamlaka ya kimsingi na kipekee.’’

Kwa upande wake Dk Ghebryeesus Tedros amesema kipaumbele chake namba moja ni uwekezaji katika afya.

image
Picha:WHO/Video Capture
( Sauti Dk Tedros)

‘‘Suala ni kwamba , sasa inabidi kutekeleza kwa vitendo. Na tatizo hapa yaweza kuwa ukosefu wa rasilimali, lakini kubwa ni ukosefu wa utashi wa kisiasa. Tukishughulikia hilo twaweza kuishi tunayoyahubiri.’’

Naye  Dk David Nabarro amesema kipaumbele chake ni afya ya jamii.

image
Picha:WHO/Video Capture
( Sauti Dk Nabarro)

‘‘Baada ya kuwa Mkurugenzi Mkuu, nitaangazia awali kabisa, katika jamii na kwenye nchi. Kwasababu uthabiti mkuu wa shirika lolote la kimataifa, hujengwa na nchi .’’

Mgombea atakayeshinda katika uchaguzi ataanza majukumu Julai Mosi, mwaka huu.