Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabilioni yahitajika kutokomeza umasikini na njaa:IFAD

Mabilioni yahitajika kutokomeza umasikini na njaa:IFAD

Dunia inahitaji kuchukua hatua haraka ili kukusanya takribani dola bilioni 265 kwa mwaka zinazohitajika kufikia malengo mawili ya maendeleo endelevu , la kutokomeza umasikini na njaa ifikapo 2030.

Hayo yamesemwa mjini Roma Italia na Kanayo F. Nwanze, Rais wa shirika la kimataifa la ufadhili wa maendeleo ya kilimo (IFAD) katika ufunguzi wa mkutano unaotafuta njia bunifu za kufadhili maendeleo vijijini .

Bwana Nwanze amesisitiza kwamba ni lazima watu kuwa wabunifu zaidi katika jinsi ya kutumia rasilimali za umma na ukusanyaji wa fedha za ufadhili na kwamba ni muhimu kuzirahisishia sekta binafsi na wadau wwngine wasio serikali njia za uwekezaji vijijini ambako kiwango cha umasikini na njaa kiko juu.

Katika mkutano huo imebainika kuwa watu wengi wa vijijini wanalima katika mashamba madogomadogo na inakadiriwa kuna pengo la dola milioni 150 baina ya ufadhili wanaohitaji na fedha zilizopo sasa.

Wajumbe wa mkutano wameafiki kwamba ili kufanikisha lengo hilo ufadhili kwa ajili ya maendeleo vijijini hauwezi kuachiwa serikali pekee bali sekta binafsi, mashirika na wadau wengine lazima washirikishwe.