Ni muhimu kuhakikisha uhakika wa chakula kwa matumizi endelevu ya maji: FAO

Ni muhimu kuhakikisha uhakika wa chakula kwa matumizi endelevu ya maji: FAO

Shirika la chakula na kilimo FAO linataka kusaidia nchi katika uzalishaji wa chakula na zaidi kwenye nchi zilizo na uhaba wa maji. Amesema hayo Dkt Pasquale Steduto ambaye ni mratibu wa mipango ya FAO wa Kanda ya Mashariki na Afrika Kaskazini (NENA) kwenye mkutano uliofanywa leo hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.  Mada iliyotamalaki kwenye mkutano huo ni maji na chakula: kupambana na uhaba wa maji katika muktadha wa maendeleo endelevu.

Dkt Pasquale amesema utekelezaji wa kilimo endelevu ni muhimu kwa mafanikio zaidi ya malengo ya maendeleo endelevu yaani SDGs na hivyo kuna uhusiano mkubwa kati ya uzalishaji wa chakula na matumizi ya maji ambayo mara nyingi haupewi kipaumbele katika sera za sekta husika. Nchi zenye maliasili ndogo kama vile maji safi zinakabiliwa na changamoto kubwa katika kuhakikisha uhakika wa chakula kwa raia wake na huwa kuna haja ya kuagiza chakula kutoka nje.

Ametaja kuwa nchi za Magharibi mwa Asia na nchi za Kaskazini mwa Afrika ni miongoni mwa nchi zenye uhaba wa maji duniani. Tayari FAO imeanzisha mradi kuhusu uhaba wa maji katika kanda hiyo kwa kutoa mfumo wa kina ili kusaidia nchi wanachama katika jitihada za kuhakikisha uhakika wa chakula na matumizi endelevu na utunzaji wa rasilimali za maji. Japokuwa mpango huo unatekelezwa katika kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini,  matokeo yake ni muhimu kwa nchi zote zinazo kabiliwa na uhaba wa maji.

(Sauti ya Pasquale)

Kilimo kina sekta mbali mbali kama vile ufugaji wa mifugo . Na mfumo wowote unaweza kufanyiwa tathmini. Kilimo kiko kwenye kipindi cha mpito kote duniani wengine wanakwenda kasi wengine pole pole. Kwa hivyo maoni yangu ni kwamba kuna nafasi ya nchi tofauti kushauriana na kufanya tathmini ya pamoja ya namna ya kulinda maji na kuongeza mifugo kwa mfano kama nchi ya Mongolia.

Wakati huo huo Dkt Pasquale amesema kuwa kilimo kina matumizi mkubwa ya maji. Hivyo, sekta hiyo ina changamoto ya kuboresha utendaji kwa matumizi ya maliasili wakati ikichangia katika uhakika wa chakula, lishe na uchumi wa vijijini.