Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunaweza kufikia dunia isiyokuwa na silaha za nyuklia - Guterres

Tunaweza kufikia dunia isiyokuwa na silaha za nyuklia - Guterres

Mkutano kwa ajili ya upokonyaji wa silaha umeanza hivi leo ikiwa ni kikao chake cha mwaka 2017 mjini Geneva, Uswisi. Ujumbe wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres uliosomwa na Mkurugenzi Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ofisi ya Geneva Michael Møller umesema kuwa ni muhimu kutatua kikamilifu na kuendeleza ukukomeshaji silaha zote za maangamizi. Bwana Guterres amesema kuwa upokonyaji wa silaha unaweza kusaidia katika jitihada za kumaliza migogoro iliyopo na kuzuia kuzuka kwa ugomvi mpya.

(Sauti ya Guterres)

"Kama Katibu Mkuu, niko imara kwa kuhakikisha kwa kikamilifu ukomeshaji wa silaha zote za maangamizi na sheria kali za silaha hizi. Nina imani tunaweza kufikia dunia isiyokuwa na silaha za nyuklia."

Ametaja chombo kinachosimamia upokonyaji wa silaha kama muhimu na kuongeza kuwa..

(Sauti ya Guterres)

"Dunia inawatazama nyinyi kama chombo cha kipekee cha kimataifa kwa uondoaji wa silaha kwa njia ya mazungumzo, kujali na ufumbuzi wa kidiplomasia, ili kukuza usalama na kuleta amani. Na kwa kujenga njia zinazoweza kukuza uaminifu na utulivu wa kimataifa. Mna jukumu kwa nchi zote na watu wote. Wakati ni sasa kulitimiza. Nawatia moyo wa kufanya kazi kwa bidii ili kupata maelewano zaidi na washirika wenu katika vyama vya kiraia na wasomi. Umoja wa Mataifa utakuwa mshirika wenu na tayari kuwasaidia vyo vyote vile."

Wengine waliozungumza kwenye kikao hicho ni Mwakilishi mkuu wa Ofisi ya upokonyaji wa silaha, Kim Won-soo na mabalozi wa nchi mbali mbali. Wote walikubaliana kuwa wakati muafaka umefika kumaliza miaka 20 ya kutokubaliana na kusonga mbele, hasa kutokana na hali ya usalama duniani na changamoto zinazoendelea kukua.