Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 1.8 Aleppo wameachwa bila huduma ya maji

Watu milioni 1.8 Aleppo wameachwa bila huduma ya maji

Wasiwasi umeendelea kuongezeka kwa takribani watu milioni 1.8 mjini Aleppo Syria ambako kumeripotiwa kuwa majeshi ya upinzani yamewakatia huduma muhimu ya maji.

Taarifa hizo kutoka ofisi ya Umoja wa mataifa ya kuratibu masuala ya dharura na misaada ya kibinadamu OCHA inasema watu Mashariki na maeneo ya vijijini Aleppo wamekuwa bila huduma ya maji kwa siku 10 sasa.

Hali hiyo inahusishwa na tatizo la kituo cha maji cha Al Khafse karibu na mji wa al-Babeneo ambalo liko chini ya udhibiti wa ISIL.

Ingawa tatizo hilo linaweza kutatuliwa, OCHA inasema haijapewa fursa ya kwenda kwenye kituo hicho ili kufanya ukarabati.

Kwingineko Syria, karibu watu milioni tano mjini Damascus bado hawana maji ya bomba kufuatia mapigano yanayoendelea yaliyoharibu miundombinu.