Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la kuongeza uwezo wa kibiashara laanza Geneva:UNCTAD

Kongamano la kuongeza uwezo wa kibiashara laanza Geneva:UNCTAD

Kwa mara ya kwanza Kamati ya Biashara na Maendeleo  ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD imeaandaa kongamano la kimataifa kwa ajili ya kuwezesha Kamati ya Kitaifa ya kurahisisha biashara, NTFCs hususan katika nchi zinazoendelea na zile zenye maendeleo duni zaidi.

Kongamano hilo lililoanza tarehe 23-27 Januari na kushirikisha pia Benki ya Dunia, Kituo cha Biashara ya Kimataifa, Shirika la Forodha Duniani na Shirika la Biashara Duniani lina lengo la kuleta mabadiliko katika nyanja ya biashara kwa kuwawezesha viongozi wa NTFCs na kuwapa fursa ya kupata msaada wa kifedha.

Baadhi ya mambo yanayojadiliwa ni jinsi ya kuunda na kuendeleza kamati hiyo, pamoja na kubadilishana uzoefu wa njia bora ya utendaji kazi na mbinu za mafunzo. Kongamano hilo pia litatoa fursa kwa NTFCs kupata msaada wa kiufundi na kusikia kutoka kwa wafadhili kuhusu msaada uliopo pamoja na kujadili changamoto zinazowakabili katika utambuzi wa vyanzo vya fedha muhimu.

Kikubwa zaidi, UNCTAD inasema nchi husika zitapata nafasi ya kufanya kazi na wafadhili wa kimataifa na wakala katika kubaini fursa hizo na kuonisha wafadhili na wahitaji.