Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uharibifu mkubwa kwa urithi wa dunia umefanywa Aleppo-UNESCO

Uharibifu mkubwa kwa urithi wa dunia umefanywa Aleppo-UNESCO

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO liliongoza ujumbe wa dharura mjini Aleppo, Syria kuanzia Januari 16 hadi 19 ili kufanya tathmini ya uharibifu katika urithi wa dunia mjini Aleppo.

Taarifa ya UNESCO imesema kuwa uharibifu mkubwa umefanywa kwenye maeneo mengi ikiwemo msikiti mkuu wa Umayyad, misikiti mingine, makanisa, madrassa na majengo mengine muhimu ya makumbusho ya kihistoria mjini Aleppo. Inakadiriwa kuwa asilimia 60% ya baadhi ya mji wa zamani umeharibiwa, na 30% kusambaratishwa kabisa.

Mkuu wa idara ya urithi wa dunia kwenye shirika la UNESCO Bi Mechtild Rossler ndiye aliyeongoza ujumbe huo huko Palmyra mwaka jana. Akizungumzia umuhimu wa maeneo hayo anasema …

(Sauti ya Rossler)

Hii ni ishara ya kujivunia ya karne ya miaka zaidi ya 2070AD, wakati malkia Chenobia alipokuwa kwenye usukani, ilikuwa ni ishara ya usanifu stadi, wa kiroho ilihali Palmyra ulikuwa mji uliowakilisha tamaduni tofauti za watu wote wa Syria.

Ujumbe huo umebaini ujasiri wa raia wa Aleppo na juhudi zilizoongozwa na wataalamu wa urithi wa dunia katika kukabiliana na vitendo hivyo wakati wa vita.

Kwa upande wa elimu, UNESCO inasema uharibifu wa taasisi za elimu  ni wa kupita kiasi.  Shule walizotembelea mashariki mwa Aleppo zimeharibiwa au zitahitaji ukarabati wa hali ya juu mfano shule ya Osam Alnadir, ambayo ni taasisi ya ufundi  mashuhuri.

Bi Ressler anatoa wito..

(Sauti ya Ressler 2)

Jukumu letu hapa ni kuhakikisha majengo yanakarabatiwa na kurejeshwa kwenye hali ya awali ni muhimu kisaikolojia kwa raia.

Cha muhimu nadhania ni kupata wadau wote wa kimataifa kuungana nasi kutusaidia na utaalamu wao na kuchangia ili kufanya ukarabati kwa hayo majengo kwa ajili ya ubinadamu.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Irina Bokova amesema uharibifu wa moja ya mji mkubwa na wa kale duniani ni janga kwa Syria. Ametoa wito wa hatua za haraka kuchukuliwa kunusuru hali hiyo huku akilaani uharibifu  mkubwa wa makavazi ya Tetrapylon na maeneo mengine ya Palmyra ambayo ilitengwa kama moja ya urithi wa dunia na UNESCO.