Skip to main content

Wagambia 45,000 waingia Senegal kukimbia sintofahamu ya kisiasa

Wagambia 45,000 waingia Senegal kukimbia sintofahamu ya kisiasa

Takribani watu 45,000 wamearifiwa kuwasili nchini Senegal kutoka Gambia kufuatia hali ya sintofahamu ya kisiasa nchini humo na kutojua nani atakayeongoza taifa hilo baada ya Rais wa zamani Yahya Jameh kuamua kutong’atuka madarakani.Grace Kaneiya na taarifa zaidi.

(TAARIFA YA GRACE)

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limetaja idadi hiyo Ijumaa mjini Geneva likisema watu hao sasa wanapatiwa hifadhi nchini Senegal ambako Adama Barrow aliapishwa kama Rais wa Gambia Alhamisi. Msemaji wa UNHCR ni Babar Baloch.

(SAUTI YA BABAR)

“Zaidi ya asilimia 75 ya waliowasili ni watoto wakiwa na wanawake. Wanaishi na jamaa wa familia au hotelini. Baadhi ya familia zinahifadhi watu 40 hadi 50, na muda si mrefu watahitaji msaada kwa sababu ya kuishiwa rasilimali”

Senegal ambayo ni jirani wa Gambia imeandaa msaada kwa ajili ya watu laki moja na UNHCR inasema iko tayari kusaidia kuorodhesha watu wanaowasili na kuratibu misaada ya kibinadamu kwa ushirikiano na serikali. Duru zinasema vikosi vikosi vya Afrika ya Magharibi vimewasili nchini Gambia Alhamisi.