Skip to main content

Japo DRC imepiga hatua kwa haki za mtoto bado kuna changamoto nyingi:CRC

Japo DRC imepiga hatua kwa haki za mtoto bado kuna changamoto nyingi:CRC

Kamati ya haki za mtoto inayoendelea na kikao chake cha 74 leo imehitimisha tafakari yake ya ripoti ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kuhusu  utekelezaji wake wa mkataba wa haki za mtoto na  ripoti yake ya awali juu ya utekelezaji wa Itifaki ya hiari ya mkataba wa uuzaji wa watoto, ukahaba  na  picha za ngono kwa watoto.

Waziri wa Haki za Binadamu wa DRC Marie-Ange Mushobekwa-Likulia akisoma ripoti hiyo ametaja baadhi ya masuala ambayo nchi yake imetekeleza ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mahakama ya vijana na vyumba vyao, pamoja na kamati ya haki za vijana ya upatanishi katika majimbo. Amesema wamefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa kupooza, wakati vifo vya watoto kutokana na malaria vimepungua kwa kiasi kikubwa na bajeti ya elimu kitaifa kuongezeka kwa asilimia 15, huku asilimia 88 ya watoto sasa wanahudhuria shule.

Ameongeza kuwa mkakati na mpango wa utekelezaji dhidi ya ukatili wa kijinsia iliyopitishwa na tangu uteuzi wa mwakilishi maalum wa kupambana na ukatili huo na uandikishaji wa watoto katika makundi yenye silaha ukatili umepungua  kwa nusu.

Pia kuna hatua kubwa iliyopigwa dhidi ya kupunguza usajili wa watoto katika vikundi vyenye silaha, tangu kusainiwa kwa mpango wa utekelezaji na Umoja wa Mataifa mwaka 2012.  Hata hivyo Kamati hiyo ya wataalam imeonyesha wasiwasi wake kuhusu hali ya watoto DRC hasa kuhusu unyanyasaji dhidi yao katika aina mbalimbali na umaskini.

Uchunguzi wa kuhitimisha ripoti hiyo  utakabidhiwa Februari 6. Kamati ya haki za mtoto itapata ripoti ya Jamhuri ya Afrika ya Kati tarehe 20 Januari.