Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mipango kabambe ya 2030 Saudia inaweza kuwa kichocheo cha haki za wanawake: UM

Mipango kabambe ya 2030 Saudia inaweza kuwa kichocheo cha haki za wanawake: UM

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu umaskini uliokithiri na haki za binadamu, Philip Alston amesema kuwa ujasiri na mipango kabambe ya kubadilisha uchumi  nchini Saudi Arabia itatoa fursa ya kipekee ya kuboresha haki za binadamu za wanawake na maskini.  Hii ni kwa mujibu wa taarifa yake baada ya ziara nchini humo hivi karibuni.

Japokuwa raia wengi wanaamini kwamba hakuna umaskini nchini humo lakini ukweli ni kwamba kuna maeneo maskini sana katika miji yote mikubwa na maeneo ya vijijini na pia kuna haja kubwa kupuuza hatma ya wakazi wengi wa muda mrefu wasio raia. Mwaka wa 2002 mwana mfalme Abdullah alikiri kuwepo kwa umaskini nchini Saudia kwa mara ya kwanza.

Mtaalamu huyo huru amesema kuna  masuala makubwa ya haki za binadamu nchini Saudi Arabia, lakini mbinu mpya kabisa ya mkakati wa  2030, programu za kitaifa hadi mwaka 2020 na fedha  vinatambua haja ya kuhamasisha ushiriki kamili wa wanawake katika soko la ajira ambalo italeta mabadiliko ya utamaduni yanayohitajika ili kuwawezesha wanawake kuwa huru zaidi katika katika uzalishaji wa  kiuchumi.

Bwana Alston ametoa wito kwa serikali kutambua hifadhi ya jamii kama haki ya binadamu ambayo amesema iko sambamba na sheria za msingi, kanuni na wajibu wa kiislamu. Na wito kwa mamlaka kutumia dira ya 2030 inayotambua haja ya kuimarisha usawa wa kijinsia katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu.  Mtaalamu huyo maalum atawasilisha ripoti ya kina na matokeo ya tathimini yake na mapendekezo kwa Baraza la Haki za Binadamu mwezi Juni 2017.