De Mistura hatimaye kushiriki katika mkutano wa Astana

De Mistura hatimaye kushiriki katika mkutano wa Astana

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amekaribisha mualiko wa mjumbe wake kuhusu masuala ya Syria, Stefan de Mistura katika mkutano wa kujadili amani nchini Syria utakaofanyika mapema wiki ijayo jijini Astana, Kazakhstan.

Mkutano huo umefadhiliwa na Urusi, Iran na Uturuki, na utahudhuriwa pia na Katibu Mkuu Guterres, ambapo amesema kuhusu suala tete la Syria ametaka mjumbe wake aiongoze timu ya Umoja wa Mataifa katika mjadala huo.

Wakati huo huo Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa, Jan Egeland, amewaambia waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi leo kuwa bado Umoja wa Mataifa hauwezi kufikisha msaada nchini Syria, kwani utekelezaji wa sitisho la mapigano yanayoendelea bado hautekelezwi katika sehemu zote.

(Sauti ya Egeland)

"Hilo lazima libadilike, na linaweza kubadilika, na ni matumaini yetu kuwa litabadilika, na nafasi ya kwanza itakuwa ni mkutano wa Astana na mimi nina furaha kwamba Urusi, Iran na Uturuki imesema katika mkutano wa leo kwamba, kama wadhamini wa mkutano wa Astana, watawahamasisha vyama ikiwa ni pamoja na serikali kuacha tabia hii yakuwazuia watoa misaada jasiri wenye uwezo na utayari kwenda katika maeneo kutoa misaada ".

Amesema mwezi Januari ndio uliomgumu zaidi katika historia ya upelekaji msaada, na vifo vya mara kwa mara katika miji minne ya Foah, Kafraya, Maday na Zabadani kwa ajili ya ukosefu wa dawa.

(Sauti ya Egeland)

"Maelfu ya familia wameyakimbia makazi yao katika mji wa Wadi barada, kuna mapigano makali, raia wengi wanauawa. Na pia ndipo kunakotegemewa katika usambazaji wa maji Damascus, hivyo sasa kwa takribani mwezi mmoja, siku 27 leo, watu milioni tano na nusu wamekosa mgao wao wa kawaida wa maji mjini Damascus. "