Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sintofahamu ya kisiasa Gambia yaathiri watoto: UNICEF

Sintofahamu ya kisiasa Gambia yaathiri watoto: UNICEF

Wakati Gambia ikiendelea kughubikwa na hali ya sintofahamu ya kisiasa hofu inazuka dhidi ya watu takribani 26,000, nusu yao wakiwa ni watoto waliokimbia nchi yao na kuingia nchi jirani ya Senegal.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF tishio la hali tete ya usalama limewaacha maelfu ya watoto nchini Gambia bila fursa ya elimu kufuatia kufungwa kwa shule nyingi katika sehemu za nchi hiyo.

Marie-Pierre Poirier mkurugenzi wa kanda ya Afrika ya Magharibi na Kati amesema dunia imejikita katika hali ya kisiasa ya Gambia, lakini imesahau maelfu ya watoto na familia zao waliojikuta katikati ya hali ya tafrani.

Ameongeza kuwa timu ya UNICEF nchini Senegal na Gambia iko tayari kuhakikisha kwamba mahitaji ya watoto yanapewa kipaumbele katika kukabiliana na hali inayoendelea kubadilika nchini Gambia.

Kwa ombi la serikali ya Senegal na washirika wa Umoja wa Mataifa, mipango ya UNICEF iko tayari kusaidia watu 40,000 kwa muda wa miezi mitatu katika huduma za afya, maji, usafi na elimu katika maeneo ya mpakani.

Pia mipango hiyo inajumuisha kupeleka wataalamu na rasilimali katika jamii zinazohifadhi wakimbizi hao ili kuwasaidia kukabiliana na wimbi la wakimbizi.