Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Facebook isitumike kusambaza hotuba za chuki Sudan Kusini

Facebook isitumike kusambaza hotuba za chuki Sudan Kusini

Mwanaharakati wa haki za wanawake nchini Sudan Kusini Betty Sunday amesema wanawake nchini humo wanawasiwasi mkubwa na hotuba za chuki hususan zile zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii.

Bi. Betty amesema hayo wakati akihojiwa na Radio Miraya ya Umoja wa Mataifa nchini humo, na kuongeza kuwa wanawake wengi wanajiunga katika kampeni dhidi ya kauli za chuki kwani wao ndio wanaoathirika zaidi na kama walezi katika kaya hawapendi kuona familia zao zikiteseka na kuchukiana kutokana na kauli hizo.

Amesema changamoto kubwa wanazokumbana nazo katika kusitisha hotuba hizo kwenye mitandao ya kijamii ni ..

(Sauti ya Betty)

"Watu hawa hawaweki majina yao ya ukweli, kwa hiyo ni kujaribu kuwatumia wahusika wa Facebook ujumbe kuwa wakikuta mtu anaweka kauli za chuki kufunga akaunti hizo, lakini ni vigumu sana, kwani unakuta mtu mmoja ana akaunti hata tano katika Facebook. Na katika kufungua mashitaka, ni nani utakaemfungulia mashitaka?, meneja wa facebook ama nani?"

Amesema tatizo halipo kwenye mitandao ya kijamii kwani madhumuni yake ni kuunganisha watu kwa uzuri, bali tatizo lipo kwa watu wenyewe, na hivyo amesisitiza umuhimu wa kila mmoja kukataa matumizi hayo mabaya.