Skip to main content

UM wakaribisha uamuzi wa kuondoa vikwazo dhidi ya Sudan

UM wakaribisha uamuzi wa kuondoa vikwazo dhidi ya Sudan

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu na vikwazo vya kimataifa Idriss Jazairy, amekaribisha uamuzi wa rais Barack Obama wa kuondoa vikwazo vingi vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Sudan.

Mtaalam huyo kupitia taarifa yake amesema uamuzi wa rais Obama umefikiwa baada ya kuona kwamba serikali ya Sudan imechukua hatua mujarabu katika muda wa miezi sita iliyopita. Aidha ametoa wito kwa mamlaka Sudan kuimarisha juhudi zao katika kuhakikisha amani na kulinda haki za binadamu nchini humo.

Uamuzi huo unafuatia mapendekezo ya mtaalam huyo katika ripoti yake kwa Baraza la haki za bindamu mwaka 2016 ambayo ilisema kwamba uwepo wa vikwazo ungeathiri biashara na uwekezaji nchini na kusababisha raia kukabiliana na changamoto katika kufurahia haki za kibinadamu.

Miongoni mwa mapendekezo ya Bwana Jazairy ilikuwa kuwepo kwa Ushrikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Sudan kwa ajili ya uagizaji wa vifaa vya tiba na dawa, pendekezo ambalo tayari limetekelezwa baada ya kupitishwa na Marekani chini ya ofisi ya Umoja wa Mataifa Khartoum kwa ushrikiano na wizara ya afya mnamo Machi 2016.

Bwana Jazairy amesema kwamba rais Obama atakumbukwa kwa kuondoa vikwazo kama hivyo pia nchini Cuba na Iran.