Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia: Ripoti mpya yaelezea ukiukwaji dhidi wavulana na wasichana

Somalia: Ripoti mpya yaelezea ukiukwaji dhidi wavulana na wasichana

Ukiukwaji mkubwa wa haki dhidi ya wavulana na wasichana ulifanywa bila kukujali katika kipindi cha miaka kadhaa nchini Somalia ikielezwa ni kutokana na uvunjaji wa sheria na utaratibu na kukosekana kwa  serikali imara. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya mpya ya ya Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa kuhusu athari za vita kwa watoto nchini Somalia .

Bi Leila Zerrougui, mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto katika migogoro ya silaha amesema hali tete ya usalama inayoendelea imeleta changamoto kubwa na wasiwasi kuhusu asili ya ukiukwaji mkubwadhidi ya watoto wa Somalia. Licha ya mazingira hayo magumu, ametaja kuwa kumekuwa na maendeleo makubwa ya kisiasa nchini humo katika kipindi cha miaka michache na hatua chanya zilizochukuliwa na Serikali ya shirikisho kwa ajili ya ulinzi wa wavulana na wasichana.

Ripoti hiyo ambayo ni ya nne ya Katibu Mkuu kuhusu watoto na migogoro ya kutumia silaha nchini Somalia kwa kipindi cha kuanzia Aprili 2010 hadi Julai 2016 imesema kuwa ukiukwaji ulifanyika kati ya 2012 na 2015 wakati wa jeshi la taifa la Somalia SNA na AMISOM walipokuwa kwenye operesheni ya pamoja ya kufurusha kikundi cha kigaidi  cha Al-Shabaab.

 Zaidi ya kesi 6,000 zilithibitishwa na Umoja wa Mataifa ikiwa asilimia 70% umetekelezwa na Al-Shabaab kwa idadi kubwa ya watoto  kutekwa, kuajiriwa, kupewa mafunzo na kutumika katika vita.  Baadhi yao walikuwa na umri wa miaka tisa na kufundishwa kutumia silaha. Watoto pia waliwekwa vizuizini na vikosi vya usalama kwa madai ya kuhatarisha usalama wa taifa ambapo Umoja wa Mataifa ulithibitisha karibu watoto 931 kati ya 2014 na Julai 2016 wakiwekwa kizuizini.

Bi Zerrougui ameongezea kuwa pamoja na hali ngumu ya usalama, serikali imefanya jitihada za kuwalinda watoto, hasa kwa kuridhia mkataba wa haki za mtoto mwaka 2015 na katika kutekeleza mipango yake.