Watoto wakimbizi kutoka Syria wapata elimu Uturuki- UNICEF

Watoto wakimbizi kutoka Syria wapata elimu Uturuki- UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema takribani watoto wakimbizi nusu milioni kutoka Syria ambao wamekimbilia Uturuki, wameandikishwa shuleni.

Naibu Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Justin Forsyth amesema hayo katika taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo akisema idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 50 tangu mwezi juni mwaka jana.

Amesema kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mzozo wa Syria, idadi ya watoto wakimbizi wa Syria huko Uturuki walioko shuleni ni kubwa kuliko ile ya ambao hawajaandikishwa, jambo ambalo amesema Uturuki inapaswa kupongezwa.

Hata hivyo amesema licha ya mafanikio hayo bado zaidi ya watoto wakimbizi 380,000 wenye umri wa kwenda shule bado hawaendi shuleni.

Kwa mantiki hiyo ametaka kuongezwa kwa rasilimali ili kuhakikisha watoto hao wanapatiwa elimu ambayo ni urithi pekee wanaoweza kutumia kukwamua nchi yao.

Uturuki inahifadhi zaidi ya watoto wakimbizi milioni moja nukta mbili, na kuifanya nchi hiyo kuongoza duniani kwa kuhifadhi kundi hilo.