Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchakato wa amani nchini Mali bado unasuasua- Annadif

Mchakato wa amani nchini Mali bado unasuasua- Annadif

Wajumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, leo wamejulishwa kuwa utekelezaji wa makubaliano ya amani na maridhiano nchini Mali bado unasuasua.

Akihutubia baraza hilo, Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa Herve Ladsous amesema ingawa kumekuwapo na mafanikio kadhaa tangu kutiwa saini kwa mkataba huo miezi 18 iliyopita, bado kuna changamoto.

Mathalani ametaja kasi ndogo ya utekelezaji wa mpango wa muda wa masuala ya usalama na kutokuwepo kwa kuaminiana baina ya pande zilizotia saini mkataba huo.

Bwana Ladsous ametaja pia mgawanyiko wa vikundi vilivyojihami kama kile cha Azawad na majaribio ya mara kwa mara ya vikundi vyenye silaha kukwamisha mkataba huo, mambo ambayo amesema yanamtia hofu iwapo wana nia ya kutekeleza, ikiwa imesalia miezi mitano ya kipindi cha mpito wa mkataba huo.

Akizungumzia hali ilivyo Mali kuhusu utekelezaji huo, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini huko, Mahamat Saleh Annadif amesema..

(Sauti ya Annadif)

“Mtu anapata hisia kuwa kuaminiana kulikowezesha kutiwa saini kwa mkataba chini ya shinikizo la jamii ya kimataiaf bado hakujaweza kuthibitishwa miongoni mwa pande zilizosaini mkataba… iwe vikundi vya waasi au serikali ya Mali. Hali ya kutoaminiana ina maana kwamba hata kama hakuna vikwazo bado kasi ni ndogo mno.”