Skip to main content

Benki ya dunia yaridhia dola milioni 450 kukwamua Yemen

Benki ya dunia yaridhia dola milioni 450 kukwamua Yemen

Benki ya dunia imetangaza mkopo wa masharti nafuu wa dola milioni 450 kwa ajili ya usaidizi wa dharura kwa ajili ya Yemen.

Naibu Rais wa benki hiyo kwa ukanda wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini Hafez Ghanem amesema fedha hizo zitaelekezewa kwenye majimbo 22 ya Yemen ambako watu wako hatarini zaidi kutokana na hali mbaya ya kibinadamu inayokumba nchi hiyo.

Mathalani amesema fedha hizo zitatumika kununua chanjo muhimu kwa watoto pamoja na lishe sambamba na kusaidia wakazi wa maeneo husika kuweza kupata huduma za msingi.

Halikadhalika zitaimarisha huduma za msingi ili kuhakikisha iwapo hali ya amani inatengamaa Yemen, wananchi wake wawe tayari kuendelea kujenga nchi yao.

Mzozo nchini Yemen umesababisha nusu ya vituo vya afya kutofanya kazi kikamilifu huku kiwango cha utapiamlo kikiwa cha juu na magonjwa yakitishia afya za wananchi.