Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO kutathmini hali ya mzozo kati ya Luba na Twa

MONUSCO kutathmini hali ya mzozo kati ya Luba na Twa

Naibu Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC David Gressly ameanza ziara ya siku tatu kwenye jimbo la Tanganyika nchini humo.

Ziara ya Bwana Gressly ambaye anawajibika na operesheni za ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini, DRC, MONUSCO upande wa mashariki mwa nchi inalenga kutathmini hali ya mzozo kati ya jamii za Luba na Twa.

Taarifa ya MONUSCO imesema pamoja na tathmini hiyo, ataangalia ni usaidizi gani unahitajika kwa mujibu wa mkataba wa amani ili kuweza kusuluhisha mzozo baina ya jamii hizo.

Kwa mantiki hiyio atakuwa na mazungumzo na mamlaka za jimbo hilo la Tanganyika pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kiraia huko Kalemie na hatimaye kutembelea maeneo ya Manono, Moba na Pweto yaliyoko pia jimboni Tanganyika.