Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yalaani shambulizi dhidi ya bunge Afghanistan

UNESCO yalaani shambulizi dhidi ya bunge Afghanistan

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, Irina Bokova, leo amelaani vikali shambulizi dhidi ya bunge mjini Kabul Afghanistan ambako watu kadhaa wamepoteza  maisha yao wakiwemo  maripota wawili wa televisheni,  Farida Mustakhdim na Noorullah. Tukio hilo lilifanyika tarehe 10 Januari mwaka huu.

Bi Bokova ameongeza kuwa analaani shambulizi kwa taasisi ambayo ni msingi wa demokrasia , mauaji ya Farida Mustakhdim na Noorullah, pamoja na watu wengine wengi ambao walikuwa wakifanya kazi kuwakilisha na kuheshimu matakwa ya watu wa Afghanistan. Amesema shambulizi hilo linakwenda kinyume na utawala bora, ambao ni muhimu kwa amani.

Farida Mustakhdim alikuwa mfanyakazi wa Wolesi Jirga televisheni, Afghanistan katika huduma za bunge ilihali Noorullah alikuwa mpiga picha wake.