Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado hujachelewa kupata chanjo ya mafua:WHO

Bado hujachelewa kupata chanjo ya mafua:WHO

Ongezeko la visa vya mafua kote duniani limechagiza wito kutoka kwa shirika la afya ulimwenguni ukiwataka watu kupata chanjo haraka iwezekanavyo.

Dr Wenqing Zhang wa shirika la afya duniani WHO, amesema kipindi cha maambukizi kimeanza mapema mwaka huu kuliko miaka mingine huku baadhi ya nchi za Ulaya na Kusini Mashariki mwa Asia zikiathirika vibaya hadi sasa.

(SAUTI DR ZHANG)

“Nadhani ujumbe wa kwanza ni rahisi, kupata chanjo, ingawa haitoshelezi lakini ndio njia bora iliyopo sasa ya kudhibiti na kujilinda na maambukizi ya mafua, watu lazima wapate chanjo sasa kama bado hawajafanya hivyo.”

Kwa mujibu wa WHO mafua husababisha vifo robo milioni kila mwaka na virusi ambavyo vimesababisha mlipuko wa sasa wa mafua ni vya H3N2.

Lakini habari njema kwa mujibu wa WHO ni kwamba mafua hayo yanaweza kudhibitiwa na dawa mbalimbali.