Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wengi wasaka hifadhi kambini kutokana na njaa Baidoa- de Clercq

Wengi wasaka hifadhi kambini kutokana na njaa Baidoa- de Clercq

Naibu Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Peter de Clercq amesema ana hofu kuwa wakazi wengi wa Baidoa, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kusini-Magharibi nchini humo watakimbia makazi yao na kusaka hifadhi kambini kutokana na ukame uliokumba eneo hilo.

Amesema hayo wakati wa ziara yake jimboni humo iliyolenga kutathmini hali halisi ya kibinadamu yanayosabishwa na ukame.

Wakati wa ziara hiyo ametembelea kambi ya wakimbizi wa ndani na hospitali kuu ya mji huo ambako alikutana na wananchi waliosaka hifadhi kambini baada ya ukame kusababisha uhaba wa maji na chakula.

Bwana de Clercq amesema takribani wasomali milioni tano nchini humo, sawa na asilimia 40 ya watu wote wanahitaji chakula baada ya uhaba wa mvua kukumba eneo kubwa la nchi hiyo.

Kwenye jimbo la Kusini-Mashariki pekee, takribani watu 820,000 wanahitaji usaidizi wa haraka wa dharura, ikiwa ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa usaidizi wa binadamu, OCHA.