Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa UM waitaka Iran kusitisha unyongaji wa vijana

Wataalamu wa UM waitaka Iran kusitisha unyongaji wa vijana

Wataalamu wa Umoja wa mataifa Jumanne wameitaka serikali ya jamhuri ya Kiislamu ya Iran kusitisha ikiwezekana mara moja unyongaji wa vijana wahalifu.

Wataalamu hao, mwakilishi maalumu kuhusu haki za binadamu Iran Asma Jahangir, mwakilishi maalumu kuhusu matumizi ya nguvu na mauaji ya kiholela Agnes Callamard na Benyam Dawit Mezmur mwenyekiti wa kamati ya haki za mtoto wamesema wanatiwa hofu na hatari inayokabili maisha ya kijana mhalifu nchini humo na kwamba huenda akanyongwa wakati wowote.

Kijana huyo alikuwa na umri wa miaka 15 alipohukumiwa kifo mwaka 2012 kwa kosa la kumchoma mtu kisu. Mnamo Februari 2014 aliruhusiwa kesi yake kusikilizwa upya kutokana na sheria mpya za kuhukumu vijana nchini humo.

Hata hivyo Juni 2015 mahakama ya uhalifu ya jimbo la Kermanshah ilibaini kwamba alikuwa amekomaa kiakili kufahamu uhalifu wake na hivyo kuthibitisha hukumu yake ya kifo na kukataa madai kwamba alitekeleza uhalifu huo katika kujitetea kufuatia jaribio la kubakwa.

Hukumu hiyo ya kifo ilizingatiwa na mahakama kuu ya Iran Agosti 2016. Iran ni miongoni mwa nchi ambazo zinaendelea kunyonga vijana licha ya hatua hiyo kupigwa marufuku na mikataba ya kimataifa ya haki za kiraia, kisiasa, haki za mtoto na za binadamu.