Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwanahabari mmoja huuawa kila baada ya siku nne: UNESCO

Mwanahabari mmoja huuawa kila baada ya siku nne: UNESCO

Jumla ya waandishi wa habari 101 waliuawa mwaka jana 2016, sawa na wastani wa mwanahabari mmoja kila baada ya siku nne limesema shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na teknolojia UNESCO.

Kwa mujibu wa ripoti kuhusu usalama wa wanahabri na hatari ya ukwepaji wa sheria iliyochapishwa Novemba 2016, idadi hiyo imepungua kilinganishwa na ile ya 2015.

Frank La Rue ambaye ni Msaidizi wa Mkurugenzi wa UNESCO kuhusu mawasiliano na taarifa amenukuliwa katika ripoti hiyo akisema tasnia hiyo iko shakani kiasi kwamba kitambulisho au kadi ya mwanataaluma au kifaa chake kinapoonekana huhalalisha kulengwa kwa mwanahabari.

Ripoti imeanika kuwa eneo hatari zaidi duniani kwa wanahabari kufanya kazi ni katika falme za Kiarabu hususani nchi zenye machafuko ambazo ni Syria, Iraq na Yemen ambapo wanahabari wangi zaidi wameuawa.

Mkurugenzi huyo amesema uhalifu dhidi ya wanahabari ukitendeka na kutochukuliwa hatua, inaonyesha kuwa vyombo vya habari vyaweza kuendelea kushambuliwa.