Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusiruhusu madhila ya 2016 kutawala 2017 Syria-UM

Tusiruhusu madhila ya 2016 kutawala 2017 Syria-UM

Wakati juhudi zikiendelea kuhakikisha utekelezazi wa usitishaji uhasama Syria, wakuu mashirika ya Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kupatikana fursa haraka bila masharti kuweza kuwafikia watoto na familia zilizoathirika ambazo bado hazifikiwi na huduma za kibinadamu nchini humo.

Wito huo umetolewa na wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa Etharin Cousin wa WFP, Anthony Lake wa UNICEF, Stephen O’Brien wa OCHA, Margaret Chan wa WHO na Filippo Grandi wa UNHCR. Wakuu hao wamesema leo hii Syria kuna maeneo 15 yanayozingirwa ambako watu takriban 700,000 wakiwemo watoto 300,000 bado wamekwama.

Huku karibu watu milioni tano wakiwemo watoto milioni mbili wanaishi katika maeneo ambayo ni vigumu kufikika na hawana huduma za kibinadamu kutokana na machafuko yanayoendelea.

Wamesisitiza kwamba madhila ya machafuko ya Syria na hasa Aleppo yanawaweka watoto katika wakati mgumu na hatari kubwa ya magonjwa na kujeruhiwa. Wametaka kuhakikisha kwamba zahma iliyoghubikwa nchi hiyo mwaka 2016 isirejee tena mwaka 2017.