Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama ya kijeshi DRC yasikiliza kesi dhidi ya wapiganaji

Mahakama ya kijeshi DRC yasikiliza kesi dhidi ya wapiganaji

Mahakama ya kijeshi huko Kamina, jimbo la Haut Lomani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imesikiliza kesi inayokabili wapiganaji wanane wanaodaiwa kuua au kuwazika hai wapiganaji 16 wa kabila la Ngiti mwezi Septemba mwaka jana. Rosemary Musumba na ripoti kamili.

(Taarifa ya Rosemary)

Katika kesi hiyo inafayofanyika chini ya ufadhili wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO, wapiganaji hao wa vikundi vya Nyatura na APCLS waliokuwa tayari wamejisalimisha kwenye jamii yadaiwa walitenda makosa hayo dhidi ya Ngiti ambao nao walikuwa ni wapiganaji waliojisalimisha.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo wakati wakiwa kwenye kituo cha kijeshi cha Kamina ambako walikuwa wanapatiwa mafunzo baada ya kusalimisha silaha zao.

Mwendesha mashtaka alieleza mahakamani kuwa wapiganaji hao wa zamani wa kabila la kihutu waliwaua au kuwazika hai kwenye kaburi moja wapiganaji 16 wa zamani wa kundi la Ngiti waliokuwepo Kamina wakisubiri kurejea nyumbani, kwa madai kuwa walikuwa wanapendelewa.

Kesi yao itaendelea Jumatano ambapo miongoni mwa mashuhuda ni mmoja wa wapiganaji ambaye alizikwa akiwa hai.