Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

G77 ni mdau muhimu kwa Umoja wa Mataifa- Guterres

G77 ni mdau muhimu kwa Umoja wa Mataifa- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema kwa kuwa ajenda 2030 ya maendeleo endelevu ni kipaumbele cha umoja huo, atashirikiana na kundi la nchi 77 kuangazia zaidi nchi zenye mahitaji.

Akihutubia kwenye hafla ya Thailand kukabidhi uenyekiti wa kundi hilo kwa Ecuador, Bwana Guterres amesema ushirikiano wa nchi za kusini utakuwa ni muhimu kuona kuwa usaidizi unaelekezwa unakotakiwa, huku akisisitiza pia ushirikiano kwenye marekebisho ya muundo wa Umoja wa Mataifa.

Akatoa pongeza kwa Thailand inayokabidhi urais wa G-77.

(Sauti ya Guterres)

Thailand imeweza kuongoza kundi hili wakati ambapo dunia imeshuhudia kupitishwa kwa mambo mawili muhimu kwa mustakhbali wa dunia hii. Mosi kuandaa na kupitishwa kwa ajenda ya maendeleo endelevu na pili ni mkataba wa mabadiliko ya tabianchi. Kundi la G77 na China chini ya uongozi wa Thailand zilikuwa na dhima muhimu kufanikisha mafanikio muhimu zaidi katika historia ya ushirikiano wa kimataifa na ningependa kupongeza Thailand kwa kazi hiyo.”

Sasa kuelekea mbele, Guterres amezungumzia utendaji wa Umoja wa Mataifa akisema marekebisho yanahitajika ikiwemo ya kimenejimenti na kiutendaji ili kuleta usawa na haki hivyo akazungumzia umuhimu wa ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na G-77 akisema ana matumaini makubwa na uongozi wa Ecuador katika chombo hicho.