Mwaka 2017 ulete unafuu Afrika Magharibi: O’Brien

Mwaka 2017 ulete unafuu Afrika Magharibi: O’Brien

Baraza la usalama limekutana leo kujadili amani na usalama barani Afrika ambapo mkutano huo umejikita katika hali kwenye ukanda wa Afrika Magharibi.

Akilihutubia baraza hilo, Mratibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa Stephen O’Brien amesema licha ya juhudi za jumuiya ya kimataifa za kukabiliana na machafuko katika ukanda huo hususani katika bonde la mto Chad bado kuna mengi ya kufanya ili kurejesha utulivu.

Amesema machafuko yanayosababishwa na kundi la kigaidi la Boko Haram yanaendelea kuathiri maelfu ya watu hususani watoto ambao wanakabiliwa na utapiamlo akitolea mfano katika jimbo la Borno nchini Nigeria ambapo zaidi ya watoto 300 wana unyafuzi.

Licha ya kadhia hizo O’Brien amesema.

( Sauti O’Brien)

Licha ya visa hivi vya kutisha , kuna tumaini kwamba mwaka 2017 huenda ukawa wenye unafuu kwa waathirika wa mgogoro kwani asili ya machafuko yanabadilika, maeneo mengi yanashikiliwa na serikali. Sasa ni wakati wa kufanya kazi kikamilifu kuongeza misaada ya kibinadamu na ulinzi pamoja na mahitaji ya misingi. Na tuweke msingi ya unafuu wa mapema na ujenzi mpya.