Idadi ya wasio na ajira 2017 kuongezeka- ILO
Shirika la kazi duniani, ILO limesema kiwango cha ukosefu wa ajira duniani kinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 0.1 mwaka huu wa 2017 kutoka asilimia 5.7 mwaka jana.
Katika ripoti yake kuhusu mwelekeo wa ajira na kijamii duniani kwa mwaka 2017, ILO imesema hali itakuwa mbaya zaidi kwa nchi za Amerika ya Kusini, Karibea na zile za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ambako idadi ya watu wenye umri wanaosaka ajira inaongezeka.
Halikadhalika ripoti inasema idadi ya wafanyakazi wanaopata ujira wa chini ya dola 3 na senti 10 kwa siku itaongezeka kwa watu milioni Tano katika miaka miwili ijayo.
Guy Rider ni Mkurugenzi Mkuu wa ILO.
(Sauti ya Rider)
"Nadhani ujumbe mkuu kwenye ripoti hii ni kwamba licha ya makadirio ya ukuaji uchumi kwa mwaka 2017, kiwango tarajiwa hakitatosha kudhibiti ongezeko la ukosefu ajira duniani.”
Kwa mantiki hiyo ILO inapendekeza pamoja usaidizi wa fedha za kuchochea uchumi na kuongezwa kwa uwekezaji wa umma kwa kuzingatia mazingira ya nchi husika ili idadi ya wasio na ajira mwaka 2018 ipungue kwa milioni mbili.