Skip to main content

Mchakato wa kisiasa Darfur bado una mkwamo- Ladsous

Mchakato wa kisiasa Darfur bado una mkwamo- Ladsous

Mapigano kwenye jimbo la Darfur nchini Sudan yamepungua kutokana na jitihada za serikali kukabili vikundi vilivyojijami, sambamba na kudhibiti mapigano baina ya makabila.

Hiyo ni kwa mujibu wa Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Herve Ladsous wakati akiwasilisha ripoti yake hali ilivyo huko Darfur mbele ya Baraza la Usalama hii leo.

Hata hivyo amesema mchakato wa kisiasa licha ya kupata nuru kufuatia bunge la Sudan kuridhia kuanzishwa kwa serikali ya maridhiano ya kitaifa bado kuna changamoto kwa kuwa..

«Kutokukwepo kwa makubaliano na serikali kuhusu muundo na yaliyomo kwenye mazungumzo ya kitaifa, vikundi vikubwa vya upinzani vinaendelea kususia mchakato wa kisiasa na kukosoa kwa kuwa wanahisi unakosa ujumuishi wa kutosha. »

Amesema wapinzani wanadai kuwa mazingira ya sasa si mazuri kwa mchakato wa maridhiano kutokana na kamatakamata ya viongozi wa upinzani na kufungwa kwa vyombo vya habari vinavyokosoa serikali.

Kuhusu vikwazo vya serikali ya Sudan dhidi ya ujumbe wa pamoja wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa, huko Darfur, UNAMID, Bwana Ladsous amesema sasa hali ni shwari kwa kuwa wanaweza kuondoa mizigo kutoka bandari ya Sudan, halikadhalika mchakato wa vibali vya wafanyakazi unafanyika vizuri.