Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP na EU wawawezesha kifedha wakimbizi Uturuki

WFP na EU wawawezesha kifedha wakimbizi Uturuki

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya EU, wanawapatia maelfu ya wakimbizi walioko Uturuki, fedha kila mwezi ili kuwawezesha kupata mahitaji muhimu kama vile chakula, kodi, dawa na mavazi ya joto.

Taarifa kuhusu mgao huo inaeleza kuwa mpango huo unatekelezwa kupitia kwa mpango wa dharura kwa usalama wa kijamii (ESSN), uliofadhiliwa na Umoja wa Ulaya.

Kundi la kwanza la kaya zilizo katika mazingira hatarishi walipokea kadi za benki na kuhamishiwa kiasi cha Euro 28 mwezi Desemba huku usajili wa wakimbizi hao ukiwa unaendelea kote nchini ili kuwezesha mpango huo wenye lengo la kuwasaidia wakimbizi milioni moja katika kipindi cha nusu ya mwaka 2017.

Wadau wengine kama vile idara ya misaada ya kibinadamu na Ulinzi (ECHO), na shirika la Msalaba mwekundu la Uturuki wanashiriki.

Uturuki ni mwenyeji kwa idadi kubwa ya wakimbizi duniani, wastani wa watu milioni tatu, ambao wengi wao walikuwa wakiyakimbia makazi yao kutoka nchi jirani ya Syria.