Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunashawishi wanawake wajifunze masuala ya anga za juu- UNOOSA

Tunashawishi wanawake wajifunze masuala ya anga za juu- UNOOSA

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya anga za juu, UNOOSA imeanza kuchukua hatua ili kuongeza idadi ya wanawake na wasichana kwenye nyanja hiyo, wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa unapigia chepuo masuala ya usawa wa kijinsia.

Mkurugenzi wa UNOOSA Simonetta Di Pippo amesema hayo akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa akisema hatua hiyo inatokana na ombi la nchi wanachama la kutaka mipango zaidi ya kuvutia wanawake katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati au STEM.

Amesema ingawa wanawake na wasichana wanahitimu hadi shahada za uzamili bado idadi yao kwenye anga za juu ni ndogo na inapungua zaidi kwenye ngazi za uongozi.

(Sauti ya Simonetta)

“Kwa hiyo tunaandaa mradi uitwao anga za juu kwa wanawake. Hivyo ningependa kuwasilisha hoja hiyo kwa nchi wanachama mwezi Juni mwaka 2018 wakati maadhimisho ya miaka 50 tangu mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa wa matumizi ya anga za juu kwa amani, UNISPACE+50. NAtumai wataunga mkono, kwa minajili ya usaidizi wa fedha ninazohitaji ili mradi ufikie kiwango ninachotaka.”

Bi. Di Pippo amesema hivi sasa anaona anawajibika kuwa mfano bora kwa wasichana na wanawake kama njia mojawapo ya kuwashawishi kujiunga na STEM na hivyo..

(Sautiya Simonetta)

“Iwapo tunatendewa sana na wanaume na tunapatiwa fursa sawa, basi ni juu yetu kuongeza bidii, kujituma ili tupate kile tunachotaka.”