Skip to main content

UNAMA yalaani mashambulizi ya Kabul na Kandahar huko Afghanistan

UNAMA yalaani mashambulizi ya Kabul na Kandahar huko Afghanistan

Umoja wa Mataifa umelaani mashambulizi yaliyofanyika hapo jana huko mjini Kabul na Kandahar ambapo watu zaidi ya 40 wameuawa, wengi wao wakiwa raia na wanadiplomasia.

Taarifa ya Ujumbe wa Umoja huo nchini Afghanistan UNAMA, imesema kuwa uhalifu huo ni kinyume cha sheria na inasikitisha kuwa mashambulizi yanasababisha mateso makubwa ya binadamu na kufanya mchakato wa amani nchini hum kuwa mgumu.

Katika shambulio la kwanza mjini Kandahar, karibu raia 13 walifariki baada ya mlipuko kutokea katika makazi ya Gavana wa jimbo hilo , wakati Gavaan huyo alipokuwa ameandaa hafla ya chakula cha jioni kwa wanadiplomasia na watu mashuhuri waliokuwa wamemtembela. Umoja wa falme za Kiarabu UAE umetangaza leo kuwa wanadiplomasia wake watano ni miongoni mwa waliokufa.

Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo.

Nako mjini Kabul, mshambuliaji wa kikundi cha kigaidi cha Taliban alijilipua nje ya jingo la bunge. Muda mfupi baadaye, kikundi hicho kililipua gari iliyokuwa na mabomu kwenye barabara kuu na kusababisha athari kwa raia kwenye basi, wafanyakazi wa ofisi za bunge, walinzi wa usalama, watu waliokuwa karibu na wauguzi waliokuwa wanahudumia majeruhi wa sambulio la kwanza.

Watu 35 walifariki na zaidi ya 50 kujeruhiwa.

Kikundi cha wanamgambo wa Taliban kimedai kililenga kurugenzi ya kitaifa ya usalama NDS katika mashambulizi hayo.

UNAMA imetaka watekelezaji wa mshambulizi hayo ya kigaidi kufikishwa katika vyombo vya sheria.