Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna nuru mazungumzo ya Cyprus- UM

Kuna nuru mazungumzo ya Cyprus- UM

Mazungumzo yenye lengo la kuunganisha kisiwa cha Cyprus kilichogawanywa mwaka 1974 kati ya raia wa Cyprus wenye asili ya Ugiriki na wale wenye asili ya Uturuki yanatia nuru na yanaweza kuwa ya kihistoria.

Espen Barth Eide ambaye ni mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye mzozo huo amesema hayo leo mjini Geneva, Uswisi akizungumza na waandishi wa habari.

(Sauti ya Espen) 

“Tuko kwenye mwelekeo sahihi na tumeshughulikia baadhi ya masuala magumu zaidi na tumetatua masuala mengi na tunakaribia kupatia suluhu baadhi ya changamoto.”

Amewapongeza Nicos Anastasiades ambaye ni kiongozi wa ujumbe wa Cyprus wa asili ya Ugiriki na Mustafa Akinci wa asili ya Uturuki kwa azma yao ya kusaka suluhu kwa zaidi ya miezi 18 sasa.

Bwana Eide amesema jitihada za sasa za kusaka suluhu zina nuru kwa kuwa mchakato unaongozwa na wananchi wenyewe wa Cyprus.

Hoja kuu ni ardhi ambapo amesema iwapo kila kitu kitaenda sawa rasimu za ramani zitawasilishwa mbele na kupitiwa na wachora ramani kutoka pande zote mbili na hatimaye kupata ramani kamili ya Cyprus.