Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maiti wabainika kwenye misitu na barafu huko Ulaya- IOM

Maiti wabainika kwenye misitu na barafu huko Ulaya- IOM

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limeelezea wasiwasi wake juu ya mazingira ya baridi kali yanayokumba maelfu ya wasaka hifadhi, wahamiaji huko Ulaya na mashariki mwa Mediteranea.

Mkurugenzi Mkuu wa IOM William Swing amesema baridi ya sasa ni kali mno kuwahi kushuhudiwa maeneo hayo wakati huu ambapo kunaripotiwa vifo vya wahamiaji kutokana na baridi kali.

Mathalani miili ya wahamiaji wawili kutoka Iraq ilibainika ikiwa imeganda kwenye msitu mmoja huko Bulgaria, huku maiti ya wahamiaji wengine wawili kutoka Afghanistan na Somalia ikipatikana huko Bulgaria na Ugiriki.

Amesema sasa wana wasiwasi zaidi kwa kuwa wahamiaji zaidi ya 15,500 hawajapata makazi ya kuweza kuhimili baridi kali ya saas huko Ugiriki, wakisubiri usajili wao kukamilika.