Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanachama wa UM wazungumzia jinsi ya kuzuia migogoro

Wanachama wa UM wazungumzia jinsi ya kuzuia migogoro

Wanachama wa Umoja wa Mataifa leo wameshiriki mjadala wa wazi wa Baraza la Usalama la Umoja huo ukiangazia uzuiaji wa migogoro na uendelezaji wa amani.

Miongoni mwa wanachama hao ni Ethiopia ambapo Waziri wake wa Mambo ya Nje Workneh Gebeyehu, amesema kwa kuzingatia changamoto za sasa za amani zinazokabili ulimwengu, kupatia kipaumbele suala la kuzuia migogoro si jambo la mbadala.

Badala yake amesema ni kwa misingi hiyo hoja ya Katibu Mkuu António Guterres ya kutumia diplomasia ya amani, inakuwa na mashiko ili kuzuia mizozo na hatimaye kuendeleza amani.

“Ni kwa mantiki hiyo, ushiriki wa dhati wa Katibu Mkuu katika diplomasia ya kuzuia mizozo, usuluhishi na kupatia mizozo suluhu kwa njia bora ya haki kupitia ofisi yake itakuwa ni jambo jema katika kushughulikia baadhi ya migogoro ambayo iko katika hali mbaya zaidi.”

Rwanda iliwakilishwa na Mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Bi. Balozi Valentine Rugwabiza ambaye amesema kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika ni njia bora zaidi ya kusaidia kuzuia na kushughulikia migogoro barani humo.

“Kufanyika kwa mashauriano ya mara kwa mara kati ya baraza la amani na usalama la Muungano wa Afrika na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji mizozo, ushughulikiana na usuluhishaji na mambo mengine ya kimkakati, kwa mtazamo wetu ni jambo muhimu sana.”