Malezi bora ya awali ni muhimu kwa maendeleo ya mtoto- UNICEF

Malezi bora ya awali ni muhimu kwa maendeleo ya mtoto- UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF leo limezindua kampeni inayolenga kuhamasisha shughuli zinazokuza ubongo wa mtoto ndani ya siku 1000 tangu anapozaliwa. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

(Taarifa ya Grace)

Kampeni hiyo iitwayo #EarlyMomentsMatter, inayoungwa mkono na taasisi ya LEGO inaeleza kuwa katika kipindi hicho, seli mpya 1000 ndani ya ubongo wa mtoto zinakutana, kasi ambayo ni ya mara moja tu katika uhai wa mtu, hivyo ikitumiwa na shughuli muhimu inasaidia maendeleo na afya ya mtoto.

UNICEF katika taarifa yake imesema ukosefu wa lishe bora, shughuli zinazochochea ubunifu, michezo, upendo na ulinzi dhidi ya ghasia vinaweza kukwamisha mkutaniko wa seli hizo na hivyo kudumaza makuzi ya mtoto.

Kupitia kampeni hiyo, UNICEF na LEGO wanashirikisha familia kwa kutumia machapisho yanayoonyesha ni kwa jinsi gani ubongo unafanya kazi pindi mtoto anapopata shughuli zinazochochea makuzi ya ubongo wake.

Kwa mantiki hiyo UNICEF inatoa wito kwa serikali kuwekeza kwenye mipango ya kumwendeleza mtoto katika siku za awali za maisha yake na kupanua wigo wa huduma za kijamii na kiafya ili wazazi na walezi waweze kupatia watoto wao.